Picha na Stella Mwaikusa
Blog hii inajaribu kuonyesha shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni zinazofanyika nchini kwetu ili kuhamasisha watu wengine kushiriki ktk shughuli hizo kwa namna moja ama nyingine katika kujikomboa kiuchumi, lakini pia inaonyesha vitu vizuri vinavyopatikana hapa kwetu ni lazima tujivunie vya kwetu.
Sunday, December 23, 2012
Tuesday, November 20, 2012
HAPA NI MNADANI DODOMA
Stella Mwaikusa
KARIBU DODOMA TUFURAHIE MINOFU
Jina la mnadani kwa wakazi wa Dodoma na
wale wanaotembelea mji huu kwa shughuli
mbalimbali za kibiashara na zile za kiserikali, na hii inatokana na umaarufu wa
eneo hili ambapo nyama za mbuzi na kuku zinachomwa na kuuzwa kwa bei nzuri.
Shughuli nzima ya kibiashara katika
sehemu hiyp hufanyika siku ya jumamosi ambapo watu wa aina mbalimbali hufika
eneo hilo na kufurahia nyama ya mbuzi na kuku huku vinywaji vikiwa vimesheheni
kusindikiza mlo huo mzuri.
Mguu wa mbuzi unauzwa kwa sh 15,000
bei ambayo watu wengi wanaonekana kuimudu kwani kwa kawaida mguu huo unaweza
kuliwa na watu wanne na zaidi hivyo kurahisha ushirika kwa maana ya
kushirikiana katika malipo, naweza kuita eneo hili na shughuli nzima ya uuzaji
wa nyama hizi kuwa ni mojawapo ya fahari ya Tanzania, karibu Dodoma.
Saturday, November 17, 2012
HUU NDIO MTO RUFIJI
Stella
Mwaikusa
KARIBU NYAMINYWIRI TUSAFIRI PAMOJA
Mto rufiji unaopatikana wilaya ya
Rufiji mkoani Pwani umekuwa na historia ndefu kwa wakazi wa kijiji cha
nyaminywiri kata ya kipugira wilayani rufiji, Kijiji cha nyaminywiri
kimegawanyika sehemu mbili kutokana na kuwepo kwa mto Rufiji.
Usafiri mkubwa wa kuwatoa wakazi
hawa kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni mtumbwi ambapo safari ya kwenda na kurudi ni sh 100 huku wanafunzi wakilipa
sh 200 kwa mwezi.
Waendesha mtumbwi wa kijiji hicho
wanasema wamekuwa wakipata taabu wakati wa masika ambapo maji huongezeka na
kulazimika kushirikiana wawili au watatu ili kuhakikisha wanaweza kuufikisha
mtumbwi pamoja na abiria salama.
Si masika tu ndio kilio na
kikwazo waendesha mitumbwi hao bali mamba na viboko ndani ya mto huo ni kikwazo kikubwa kwani wamekuwa
wakipambana na viboko hasa wanapokuwa wamezaa kwani kiboko anapokuwa na mtoto
basi kila mtumbwi unapopita karibu na mwanae huleta vurugu kwa kupindua mtumbwi
na kuleta madhara, wanasema mwaka 2010 kiboko alipindua mtumbwi na kusababisha
vifo vya watoto 9 wanafunzi wa shule ya nyaminywiri.
Friday, November 16, 2012
KARIBU UTETE
Stella Mwaikusa
KARIBU UTETE TUVUKE NA MV
UTETE
MV Utete ni kivuko kinachopatikana katika wilaya ya Rufiji mkoani pwani na
kinafanya kazi zake Mto rufiji ambapo
wakazi wa utete hutumia kivuko hicho kwenda ng’ambo ya pili sehemu zenye
mashamba na makazi ya watu.
Kivuko hicho pia kimekuwa kikiwavusha wanafunzi wanaoishi
vijiji vya Luwe na mkongo wanaosoma utete wilayani na kuwa msaada mkubwa wa
kuvusha magari kutoka Ng’ambo ya pili na kwenda wilayani utete ambako huduma
nyingi za kijamii zinapatikana ikiwemo hospitali, ofisi mbalimbali za kiserikali,
shule na vyuo.
“ Kivuko kinasaidia sana pale tunapokuwa na mgonjwa kwa
sababu kuzunguka na gari la wagonjwa mpaka kibiti ni mbali lakini tukipita hapa
ni rahisi kumfikisha mgonjwa hospital ya wilaya kwa wakati” Anaeleza Tarcis Bwakila Mganga mkuu wa kituo cha afya
cha Nyaminywiri.
Kivuko hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa vijiji vya
Luwe, Mkongo,Nyaminywiri na utete wialayani pia imewarahisishia waendesha
pikipiki wa Ikwiriri ambao hutumia kivuko hicho kuvusha pikipiki zao kwani
wanasema njia hiyo ya mkongo kupitia mto rufiji ni njia ya mkato.
Kivuko hicho kina miaka mitatu tangu kianze kufanya kazi zake
na watumiaji wa kivuko hicho wanasema wanamshukuru Mbunge wao wa zamani Dk
Mtulya ambaye alisimamia kikamilifu kuhakikisha kivuko hicho kinakuwepo hapo.
Bei za kivuko kwa abiria ni sh 200 huku magari yakivushwa kwa
shilingi 500 na kwa sasa kivuko hicho
hakivushi hii ni kutokana na kina cha maji cha mto rufiji kupungua na
michanga kujaa hali inayofanya kishindwe kufanya kazi zake kikamilifu.
Thursday, November 15, 2012
MAAJABU YA BWAWA LA ZUMBI
Stella Mwaikusa
BWAWA LA ZUMBI LIMEIFANYA NYAMINYWIRI KUWA SELOU NDOGO
Kijiji cha
nyaminywiri kinapatikana katika kata ya kipugira wilayani Rufiji katika mkoa wa
Pwani, ni umbali wa kilomita 30 kutoka mbuga za wanyama za Selou ni mwendo wa nusu saa kuufikia mji wa
kibiashara na sehemu wanayofikia watalii wanaotembelea mbuga za Selou mji wa
Mloka.
Wakazi wa kijiji hiki
wanajishughulisha na kilimo cha Mpunga, mahindi, mbogamboga na Kilimo cha
korosho zao kuu la biashara kwa wakazi hao blla kusahau biashara ya samaki
kutokana na kijiji hiki kuzungukwa na maji ya mto Rufiji na Bwawa kubwa la
Zumbi ambalo ndio linakifanya kijiji hiki kuwa Selou ndogo.
Bwawa la Zumbi lina
historia ndefu katika kijiji cha Nyaminwiri kwani wenyeji wanasema kila kijana
anayetaka kazi ya uvuvi basi huanza kujifunzia katika Bwawa hilo kutokana na
wingi wa samaki wanaopatikana humo ambapo kijana yeyote hujisikia faraja baada
ya kuanza kazi na kupata mafanikio yaani kupata samaki wa kutosha
Unapofika katka bwawa
hili huwezi kuamini kama kuna kiumbe hai anaishi humo kwani maji yake ni tulivu
na yana rangi ambayo ni vigumu kuitambua kwani unapoyaangalia yanaonekana kama
yamefubaa au yana rangi ya kijani hivi, lakini ukiyachota kwenye chombo basi
yana rangi ya kawaida.
Nilipotaka kujua
ukimya wa bwawa lile mwenyeji wangu alinijibu kwamba hiyo ni ishara ya
kuonyesha ni kuwa bwawa hilo lina kina kirefu sana hivyo akakiri kwamba hata
wao huvua wakiwa kwenye mitumbwi kutokana na ukweli kwamba bwawa hilo lina chatu
wakubwa na mamba ambao inasemekana ni wakubwa kuliko mamba wote wanaopatikana
duniani.
Ndani ya bwawa hili wanapatikana samaki wa aina mbalimbali kama vile Kumba,kasa,panga panga, kitoga na Kambale wote wakipatikana kwa misimu tofauti kwa mfano mwezi huu wa oktoba samaki aina ya kumba ndio wanaopatikana kwa wingi na wenyeji wanasema samaki wanaopatikana katika bwawa hilo ni watamu kuliko wale wa mto Rufiji
KICHUGUU CHA AJABU RUFIJI
Stella
Mwaikusa
Nilipotembelea
Rufiji niliona vitu vingi vya kupendeza ambavyo naweza kuviita ni fahari ya
Tanzania ikiwemo mito, mabwawa na mapori yaliyojaa wanyama wa kila aina lakini
kikubwa zaidi ni kichuguu ambacho kipo katikati ya nyumba za wenyeji wa
kijijiji cha nyaminywiri.
Kichuguu
hiki kimedumu kwa zaidi ya miaka 30 huku mvua na jua havijaweza kukitikisa
kichuguu hiki ambacho kinapatikana katika kijiji cha nyaminywiri kata ya
kipugira wilaya ya rufiji, wenyeji wa kijiji hiki wamekuwa wakipumzika Karibu
na kichuguu
Wanasema
hawajawahi kuona udongo ukitoka hata mvua kubwa ikinyesha lakini pia wanasema
hawajawahi kuona mchwa wanaotengeneza zaidi ya kusikia sauti ya kutembea kwa
wadudu kutokea ndani ya kichuguu hicho ambao wanaaminika kuwa ni mchwa.
“Sisi
tunaona kama ni kitu cha kawaida tu maana tumezaliwa na kukikuta kichuguu hiki
na limekuwa eneo letu la kupumzika" anaeleza” Bi Siyenu Abdalah na
kuongeza kuwa kichuguu hiki kimekuwa kama moja ya alama na utamaduni wa eneo
hilo la nyaminywiri.
Binafsi
naweza kusema kichuguu hiki ni utalii wetu wa ndani ambao bado haujambulika ni
jukumu la viongozi wa vijiji na kata kutambua fursa za utalii zilizopo katika
maeneo yao.
Pamoja
na kuwepo kwa kichuguu hicho kijiji cha nyaminywiri kina vivutio vingi ikiwa ni
pamoja Bwawa kubwa ambalo linazungukwa na msitu mkubwa uliojaa wanyama wa kila
aina wakiwemo simba, chui, Tembo na nyoka aina ya chatu.
Subscribe to:
Posts (Atom)