Tuesday, November 20, 2012

HAPA NI MNADANI DODOMA



                                     


                                 Stella Mwaikusa    
        
                         KARIBU DODOMA TUFURAHIE MINOFU

Jina la mnadani kwa wakazi wa Dodoma na wale wanaotembelea mji  huu kwa shughuli mbalimbali za kibiashara na zile za kiserikali, na hii inatokana na umaarufu wa eneo hili ambapo nyama za mbuzi na kuku zinachomwa na kuuzwa kwa bei nzuri.

Shughuli nzima ya kibiashara katika sehemu hiyp hufanyika siku ya jumamosi ambapo watu wa aina mbalimbali hufika eneo hilo na kufurahia nyama ya mbuzi na kuku huku vinywaji vikiwa vimesheheni kusindikiza mlo huo mzuri.

Mguu wa mbuzi unauzwa kwa sh 15,000 bei ambayo watu wengi wanaonekana kuimudu kwani kwa kawaida mguu huo unaweza kuliwa na watu wanne na zaidi hivyo kurahisha ushirika kwa maana ya kushirikiana katika malipo, naweza kuita eneo hili na shughuli nzima ya uuzaji wa nyama hizi kuwa ni mojawapo ya fahari ya Tanzania, karibu Dodoma.

Saturday, November 17, 2012

HUU NDIO MTO RUFIJI


                                                                                     

                                                                    Stella Mwaikusa                           
                                      
                                         KARIBU NYAMINYWIRI TUSAFIRI PAMOJA
Mto rufiji unaopatikana wilaya ya Rufiji mkoani Pwani umekuwa na historia ndefu kwa wakazi wa kijiji cha nyaminywiri kata ya kipugira wilayani rufiji, Kijiji cha nyaminywiri kimegawanyika sehemu mbili kutokana na kuwepo kwa mto Rufiji.

Usafiri mkubwa wa kuwatoa wakazi hawa kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni mtumbwi ambapo safari ya kwenda  na kurudi ni sh 100 huku wanafunzi wakilipa sh 200 kwa mwezi.
Waendesha mtumbwi wa kijiji hicho wanasema wamekuwa wakipata taabu wakati wa masika ambapo maji huongezeka na kulazimika kushirikiana wawili au watatu ili kuhakikisha wanaweza kuufikisha mtumbwi pamoja na abiria salama.


Si masika tu ndio kilio na kikwazo waendesha mitumbwi hao bali mamba na viboko ndani ya  mto huo ni kikwazo kikubwa kwani wamekuwa wakipambana na viboko hasa wanapokuwa wamezaa kwani kiboko anapokuwa na mtoto basi kila mtumbwi unapopita karibu na mwanae huleta vurugu kwa kupindua mtumbwi na kuleta madhara, wanasema mwaka 2010 kiboko alipindua mtumbwi na kusababisha vifo vya watoto 9 wanafunzi wa shule ya nyaminywiri.

Friday, November 16, 2012

KARIBU UTETE


                                                            Stella Mwaikusa
                                          
                                       KARIBU UTETE TUVUKE NA MV UTETE

MV Utete ni kivuko kinachopatikana  katika wilaya ya Rufiji mkoani pwani na kinafanya kazi zake  Mto rufiji ambapo wakazi wa utete hutumia kivuko hicho kwenda ng’ambo ya pili sehemu zenye mashamba na makazi ya watu.

Kivuko hicho pia kimekuwa kikiwavusha wanafunzi wanaoishi vijiji vya Luwe na mkongo wanaosoma utete wilayani na kuwa msaada mkubwa wa kuvusha magari kutoka Ng’ambo ya pili na kwenda wilayani utete ambako huduma nyingi za kijamii zinapatikana ikiwemo hospitali, ofisi mbalimbali za kiserikali, shule na vyuo.

“ Kivuko kinasaidia sana pale tunapokuwa na mgonjwa kwa sababu kuzunguka na gari la wagonjwa mpaka kibiti ni mbali lakini tukipita hapa ni rahisi kumfikisha mgonjwa hospital ya wilaya kwa wakati” Anaeleza  Tarcis Bwakila Mganga mkuu wa kituo cha afya cha Nyaminywiri.

Kivuko hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa vijiji vya Luwe, Mkongo,Nyaminywiri na utete wialayani pia imewarahisishia waendesha pikipiki wa Ikwiriri ambao hutumia kivuko hicho kuvusha pikipiki zao kwani wanasema njia hiyo ya mkongo kupitia mto rufiji ni njia ya mkato.

Kivuko hicho kina miaka mitatu tangu kianze kufanya kazi zake na watumiaji wa kivuko hicho wanasema wanamshukuru Mbunge wao wa zamani Dk Mtulya ambaye alisimamia kikamilifu kuhakikisha kivuko hicho kinakuwepo hapo.

Bei za kivuko kwa abiria ni sh 200 huku magari yakivushwa kwa shilingi 500 na kwa sasa kivuko hicho  hakivushi hii ni kutokana na kina cha maji cha mto rufiji kupungua na michanga kujaa hali inayofanya kishindwe kufanya kazi zake kikamilifu.

Thursday, November 15, 2012

MAAJABU YA BWAWA LA ZUMBI




                                                     
                                                  
  



                                             Stella Mwaikusa

BWAWA LA ZUMBI LIMEIFANYA NYAMINYWIRI KUWA SELOU NDOGO

Kijiji cha nyaminywiri kinapatikana katika kata ya kipugira wilayani Rufiji katika mkoa wa Pwani, ni umbali wa kilomita 30 kutoka mbuga za wanyama za Selou  ni mwendo wa nusu saa kuufikia mji wa kibiashara na sehemu wanayofikia watalii wanaotembelea mbuga za Selou mji wa Mloka.

Wakazi wa kijiji hiki wanajishughulisha na kilimo cha Mpunga, mahindi, mbogamboga na Kilimo cha korosho zao kuu la biashara kwa wakazi hao blla kusahau biashara ya samaki kutokana na kijiji hiki kuzungukwa na maji ya mto Rufiji na Bwawa kubwa la Zumbi ambalo ndio linakifanya kijiji hiki kuwa Selou ndogo.

Bwawa la Zumbi lina historia ndefu katika kijiji cha Nyaminwiri kwani wenyeji wanasema kila kijana anayetaka kazi ya uvuvi basi huanza kujifunzia katika Bwawa hilo kutokana na wingi wa samaki wanaopatikana humo ambapo kijana yeyote hujisikia faraja baada ya kuanza kazi na kupata mafanikio yaani kupata samaki wa kutosha

Unapofika katka bwawa hili huwezi kuamini kama kuna kiumbe hai anaishi humo kwani maji yake ni tulivu na yana rangi ambayo ni vigumu kuitambua kwani unapoyaangalia yanaonekana kama yamefubaa au yana rangi ya kijani hivi, lakini ukiyachota kwenye chombo basi yana rangi ya kawaida.

Nilipotaka kujua ukimya wa bwawa lile mwenyeji wangu alinijibu kwamba hiyo ni ishara ya kuonyesha ni kuwa bwawa hilo lina kina kirefu sana hivyo akakiri kwamba hata wao huvua wakiwa kwenye mitumbwi kutokana na ukweli kwamba bwawa hilo lina chatu wakubwa na mamba ambao inasemekana ni wakubwa kuliko mamba wote wanaopatikana duniani.
 
Ndani ya bwawa hili wanapatikana samaki wa aina mbalimbali kama vile Kumba,kasa,panga panga, kitoga na  Kambale wote wakipatikana kwa misimu tofauti kwa mfano mwezi huu wa oktoba samaki aina ya kumba ndio wanaopatikana kwa wingi na wenyeji wanasema samaki wanaopatikana katika bwawa hilo  ni watamu kuliko wale wa mto Rufiji

KICHUGUU CHA AJABU RUFIJI

 

                                   Stella Mwaikusa
Nilipotembelea Rufiji niliona vitu vingi vya kupendeza ambavyo naweza kuviita ni fahari ya Tanzania ikiwemo mito, mabwawa na mapori yaliyojaa wanyama wa kila aina lakini kikubwa zaidi ni kichuguu ambacho kipo katikati ya nyumba za wenyeji wa kijijiji cha nyaminywiri.
Kichuguu hiki kimedumu kwa zaidi ya miaka 30 huku mvua na jua havijaweza kukitikisa kichuguu hiki ambacho kinapatikana katika kijiji cha nyaminywiri kata ya kipugira wilaya ya rufiji, wenyeji wa kijiji hiki wamekuwa wakipumzika Karibu na kichuguu
Wanasema hawajawahi kuona udongo ukitoka hata mvua kubwa ikinyesha lakini pia wanasema hawajawahi kuona mchwa wanaotengeneza zaidi ya kusikia sauti ya kutembea kwa wadudu kutokea ndani ya kichuguu hicho ambao wanaaminika kuwa ni mchwa.
“Sisi tunaona kama ni kitu cha kawaida tu maana tumezaliwa na kukikuta kichuguu hiki na limekuwa eneo letu la kupumzika" anaeleza” Bi Siyenu Abdalah na kuongeza kuwa kichuguu hiki kimekuwa kama moja ya alama na utamaduni wa eneo hilo la nyaminywiri.
Binafsi naweza kusema kichuguu hiki ni utalii wetu wa ndani ambao bado haujambulika ni jukumu la viongozi wa vijiji na kata kutambua fursa za utalii zilizopo katika maeneo yao.

Pamoja na kuwepo kwa kichuguu hicho kijiji cha nyaminywiri kina vivutio vingi ikiwa ni pamoja Bwawa kubwa ambalo linazungukwa na msitu mkubwa uliojaa wanyama wa kila aina wakiwemo simba, chui, Tembo na nyoka aina ya chatu.