Sunday, March 10, 2013

Tembelea makumbusho ya Mwalimu Nyerere yaliyopo Butiama

 Hii ni  Redio ambayo alikuwa akiitumia baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere  enzi ya uhai wake..
                                                                 Hii ni ngoma ya wazanaki
                                         Buti alizokuwa akitumia baba wa Taifa katika kazi za shamba.
                                      Kiti alichokuwa anakalia Mwalimu Julius Nyerere enzi ya uhai wake

Friday, March 8, 2013

Karibu Bunda



                                              
                                                  mtoto akichunga ng'ombe  katika kijiji cha Nyabehu
                                                 mtoto akitimua mbio baada ya kuulizwa jina lake
                          mama akichunga ng'ombe ni Nyabehu hiyo    
                              
                                    
                                         Na  Stella Mwaikusa           

                                   Guta mpaka Nyabehu hiyo…….

Mimi na waandishi wenzangu, tulitembelea  katika kijiji cha Guta,  Kinyambwiga na Nyabehu, vijiji  vinavyopatikana katika kata ya Guta wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Tulishuhudia mambo ya kufurahisha na mengine yalitupa maswali, lakini kwa ujumla tuliifurahia safari, kati ya mambo tuliyoyaona ni kuwakuta akina mama wakichunga kundi kubwa la ng’ombe na mbuzi kitu ambacho si cha kawaida sana katika jamii nyingi za kitanzania.

Kitu kingine tulichokishuhudia ni kuona mtoto wa kiume wa miaka minne akichunga kundi la ng’ombe wanaokadirwa kuwa hamsini mpaka sitini, na tulipojaribu kumuuliza anawezaje kulidhibiti kundi lile,  haikuwa rahisi kwetu kwani hatukuweza kuongea lugha ya kikurya ambayo ndiyo pekee anayoifahamu.

Lakini baada ya kuona mwandishi mwingine akishuka kwenye gari mtoto alikimbia na kuwaacha ngombe wakizagaa, hali ambayo ilitushangaza kwani hatukujua sababu iliyomkimbiza na tukaamua kuondoka.

Tukiwa tunaendelea na safari ya kuelekea kijiji cha Nyabehu kitongoji cha Nyantare, tulisimamisha gari ili kuwauliza wenyeji ambao walikuwa nje ya nyumba yao iliyozungushiwa wigo wa katani na miti ya miiba, hali ambayo haikuwa rahisi kwetu kuingia ndani ya wigo huo.

Dereva akajaribu kuita ili aweze kuzungumza nao, lakini ghafla wasichana wawili wanaokadiriwa kuwa na miaka 13-15 pamoja na mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na miaka sita hivi, wote watatu wakakakimbilia ndani ya nyumba yao.

Tukaanza kujiuliza kwa nini hali ile ya watoto kukimbia inajirudia tena, lakini tukiwa katika hali ya kujiuliza, ghafla akajitokeza mama kutoka ndani na akasikiliza shida yetu, akutuelekeza, na tulipotaka kujua kwa nini watoto walikimbilia ndani ndipo tukapata kisa.

“Huku kwetu kuna vikundi vinavyofanya mauaji vinaitwa makirikiri ndiyo maana watoto wakiona gari linasimama maeneo ya huku kwetu wanahisi huenda ndio hao” anaeleza.

Tukaifahamu sababu ya kukimbia  kwa yule mtoto aliyekuwa akichunga, kwani hata tulipokuwa tunarudi tulijaribu kusimaisha gari ili kumsaidia mama aliyekuwa na mtoto akitokea kliniki huku jua likiwaka sana.

Kama ilivyokuwa kwa wale wengine, mama yule alikataa kabisa kupewa lifti, tukaamua kuondoka  maana tayari tulishaambiwa sababu., tembelea Bunda ni sehemu yenye vyakula vingi, kuna samaki, nyama za ng’ombe na mbuzi na maziwa kibao bila kusahau kichuri.

Tuesday, November 20, 2012

HAPA NI MNADANI DODOMA



                                     


                                 Stella Mwaikusa    
        
                         KARIBU DODOMA TUFURAHIE MINOFU

Jina la mnadani kwa wakazi wa Dodoma na wale wanaotembelea mji  huu kwa shughuli mbalimbali za kibiashara na zile za kiserikali, na hii inatokana na umaarufu wa eneo hili ambapo nyama za mbuzi na kuku zinachomwa na kuuzwa kwa bei nzuri.

Shughuli nzima ya kibiashara katika sehemu hiyp hufanyika siku ya jumamosi ambapo watu wa aina mbalimbali hufika eneo hilo na kufurahia nyama ya mbuzi na kuku huku vinywaji vikiwa vimesheheni kusindikiza mlo huo mzuri.

Mguu wa mbuzi unauzwa kwa sh 15,000 bei ambayo watu wengi wanaonekana kuimudu kwani kwa kawaida mguu huo unaweza kuliwa na watu wanne na zaidi hivyo kurahisha ushirika kwa maana ya kushirikiana katika malipo, naweza kuita eneo hili na shughuli nzima ya uuzaji wa nyama hizi kuwa ni mojawapo ya fahari ya Tanzania, karibu Dodoma.

Saturday, November 17, 2012

HUU NDIO MTO RUFIJI


                                                                                     

                                                                    Stella Mwaikusa                           
                                      
                                         KARIBU NYAMINYWIRI TUSAFIRI PAMOJA
Mto rufiji unaopatikana wilaya ya Rufiji mkoani Pwani umekuwa na historia ndefu kwa wakazi wa kijiji cha nyaminywiri kata ya kipugira wilayani rufiji, Kijiji cha nyaminywiri kimegawanyika sehemu mbili kutokana na kuwepo kwa mto Rufiji.

Usafiri mkubwa wa kuwatoa wakazi hawa kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni mtumbwi ambapo safari ya kwenda  na kurudi ni sh 100 huku wanafunzi wakilipa sh 200 kwa mwezi.
Waendesha mtumbwi wa kijiji hicho wanasema wamekuwa wakipata taabu wakati wa masika ambapo maji huongezeka na kulazimika kushirikiana wawili au watatu ili kuhakikisha wanaweza kuufikisha mtumbwi pamoja na abiria salama.


Si masika tu ndio kilio na kikwazo waendesha mitumbwi hao bali mamba na viboko ndani ya  mto huo ni kikwazo kikubwa kwani wamekuwa wakipambana na viboko hasa wanapokuwa wamezaa kwani kiboko anapokuwa na mtoto basi kila mtumbwi unapopita karibu na mwanae huleta vurugu kwa kupindua mtumbwi na kuleta madhara, wanasema mwaka 2010 kiboko alipindua mtumbwi na kusababisha vifo vya watoto 9 wanafunzi wa shule ya nyaminywiri.

Friday, November 16, 2012

KARIBU UTETE


                                                            Stella Mwaikusa
                                          
                                       KARIBU UTETE TUVUKE NA MV UTETE

MV Utete ni kivuko kinachopatikana  katika wilaya ya Rufiji mkoani pwani na kinafanya kazi zake  Mto rufiji ambapo wakazi wa utete hutumia kivuko hicho kwenda ng’ambo ya pili sehemu zenye mashamba na makazi ya watu.

Kivuko hicho pia kimekuwa kikiwavusha wanafunzi wanaoishi vijiji vya Luwe na mkongo wanaosoma utete wilayani na kuwa msaada mkubwa wa kuvusha magari kutoka Ng’ambo ya pili na kwenda wilayani utete ambako huduma nyingi za kijamii zinapatikana ikiwemo hospitali, ofisi mbalimbali za kiserikali, shule na vyuo.

“ Kivuko kinasaidia sana pale tunapokuwa na mgonjwa kwa sababu kuzunguka na gari la wagonjwa mpaka kibiti ni mbali lakini tukipita hapa ni rahisi kumfikisha mgonjwa hospital ya wilaya kwa wakati” Anaeleza  Tarcis Bwakila Mganga mkuu wa kituo cha afya cha Nyaminywiri.

Kivuko hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa vijiji vya Luwe, Mkongo,Nyaminywiri na utete wialayani pia imewarahisishia waendesha pikipiki wa Ikwiriri ambao hutumia kivuko hicho kuvusha pikipiki zao kwani wanasema njia hiyo ya mkongo kupitia mto rufiji ni njia ya mkato.

Kivuko hicho kina miaka mitatu tangu kianze kufanya kazi zake na watumiaji wa kivuko hicho wanasema wanamshukuru Mbunge wao wa zamani Dk Mtulya ambaye alisimamia kikamilifu kuhakikisha kivuko hicho kinakuwepo hapo.

Bei za kivuko kwa abiria ni sh 200 huku magari yakivushwa kwa shilingi 500 na kwa sasa kivuko hicho  hakivushi hii ni kutokana na kina cha maji cha mto rufiji kupungua na michanga kujaa hali inayofanya kishindwe kufanya kazi zake kikamilifu.