mtoto akitimua mbio baada ya kuulizwa jina lake
mama akichunga ng'ombe ni Nyabehu hiyo
Na Stella Mwaikusa
Guta mpaka Nyabehu hiyo…….
Mimi na waandishi wenzangu, tulitembelea katika kijiji cha Guta, Kinyambwiga na Nyabehu, vijiji vinavyopatikana katika kata ya Guta wilaya ya
Bunda mkoani Mara.
Tulishuhudia mambo ya kufurahisha na mengine yalitupa maswali, lakini kwa ujumla tuliifurahia safari, kati ya mambo tuliyoyaona ni kuwakuta akina mama wakichunga kundi kubwa la ng’ombe na mbuzi kitu ambacho si cha kawaida sana katika jamii nyingi za kitanzania.
Kitu kingine tulichokishuhudia ni kuona mtoto wa kiume wa
miaka minne akichunga kundi la ng’ombe wanaokadirwa kuwa hamsini mpaka sitini,
na tulipojaribu kumuuliza anawezaje kulidhibiti kundi lile, haikuwa rahisi kwetu kwani hatukuweza kuongea
lugha ya kikurya ambayo ndiyo pekee anayoifahamu.
Lakini baada ya kuona mwandishi mwingine akishuka kwenye gari
mtoto alikimbia na kuwaacha ngombe wakizagaa, hali ambayo ilitushangaza kwani
hatukujua sababu iliyomkimbiza na tukaamua kuondoka.
Tukiwa tunaendelea na safari ya kuelekea kijiji cha Nyabehu
kitongoji cha Nyantare, tulisimamisha gari ili kuwauliza wenyeji ambao walikuwa
nje ya nyumba yao iliyozungushiwa wigo wa katani na miti ya miiba, hali ambayo
haikuwa rahisi kwetu kuingia ndani ya wigo huo.
Dereva akajaribu kuita ili aweze kuzungumza nao, lakini
ghafla wasichana wawili wanaokadiriwa kuwa na miaka 13-15 pamoja na mtoto wa
kiume anayekadiriwa kuwa na miaka sita hivi, wote watatu wakakakimbilia ndani
ya nyumba yao.
Tukaanza kujiuliza kwa nini hali ile ya watoto kukimbia
inajirudia tena, lakini tukiwa katika hali ya kujiuliza, ghafla akajitokeza
mama kutoka ndani na akasikiliza shida yetu, akutuelekeza, na tulipotaka kujua
kwa nini watoto walikimbilia ndani ndipo tukapata kisa.
“Huku kwetu kuna vikundi vinavyofanya mauaji vinaitwa
makirikiri ndiyo maana watoto wakiona gari linasimama maeneo ya huku kwetu
wanahisi huenda ndio hao” anaeleza.
Tukaifahamu sababu ya kukimbia kwa yule mtoto aliyekuwa akichunga, kwani
hata tulipokuwa tunarudi tulijaribu kusimaisha gari ili kumsaidia mama
aliyekuwa na mtoto akitokea kliniki huku jua likiwaka sana.
Kama ilivyokuwa kwa wale wengine, mama yule alikataa kabisa
kupewa lifti, tukaamua kuondoka maana
tayari tulishaambiwa sababu., tembelea Bunda ni sehemu yenye vyakula vingi,
kuna samaki, nyama za ng’ombe na mbuzi na maziwa kibao bila kusahau kichuri.
No comments:
Post a Comment